Marehemu Bi Kidude alikuwa ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika.
Jina lake halisi ni Fatuma binti Baraka. Bi Kidude ni msanii mkongwe na mahiri
sana katika fani ya muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina
la Taarabu.
Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki
toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrikaumekita
sana katika mwambao wa Afrika
Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Leo hii ni Marehemu! Nguli na Mtunukiwa wa
Nishani ya Uhuru wa Tanganyika/Tanzania 2012, Fatuma binti Baraka au Bi Kidude,
alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia
ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara
wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi Kidude aliwahi kusimulia kuwa hafahamu
tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa
wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla
ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata
taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya
miaka 90.
Bi Kidude aliendelea kusema uimbaji aliuanza
tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe
na aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad. Anasema wageni wengi kutoka
sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi
Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale
nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye
kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku
nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba.
Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza
alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya
kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa
ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo
aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930,
huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini
ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na
shughuli zake uimbaji.
Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba,
kwani pia ni mfanyabiashara ya 'wanja' na 'hina' ambavyo
anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za
mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na
ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna
aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana
upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira
yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote
akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba
ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria
hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa
kama Mtanzania na si kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo
alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude
anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana
ikiwa ni pamoja
na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja
na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo
ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa
Jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata
elimu nyingine zaidi ya Kurani.
Bi Kidude pia amekuwa akishirikishwa na wasanii
wengi wakongwe na chipukizi katika nyimbo zao. Miongoni mwa nyimbo zinazotamba
sana siku hizi ambazo Bi Kifude ameimba na vijana wa kisasa ni za Msanii Ali
Toll maarufu AT.
Mbali na AT lakini pia Bi Kidude amewika na
kung'ara zaidi katika wimbo mwingine wa vijana wa Ahmada Umelewa wa
Msanii Offside Trick ambao umepigwa marufuku kupigwa kwa sasa visiwani
Zanzibar.
R.I.P FATUMA BARAKA “BI KIDUDE”..
Kwa hisani kubwa ya mrokim
No comments:
Post a Comment
aminaplummer20@gmail.com